Msanii maarufu kutoka Marekani, Sean “Diddy” Combs, amehukumiwa kifungo cha miezi 50 jela, sawa na miaka minne na miezi miwili, baada ya kukutwa na hatia ya makosa mawili yanayohusiana na usafirishaji wa watu kwa ajili ya biashara ya ukahaba.
Katika mashtaka hayo, Diddy alihusishwa na kuwapeleka wapenzi wake wa zamani, Cassie Ventura na Jane, ili washiriki ngono na wanaume waliolipwa kwenye sherehe zilizojulikana kama “Freak Offs”.
Diddy alikamatwa Septemba 16, 2024, katika hoteli ya Park Hyatt, Manhattan – New York, na kisha kupelekwa moja kwa moja katika gereza la Metropolitan.
Kesi yake ilianza kusikilizwa Mei 5, 2025, ambapo mashahidi mbalimbali waliitwa kutoa ushahidi akiwemo mpenzi wake wa muda mrefu Cassie Ventura, Jane, Mia, Kid Cudi, Bongolani, pamoja na mama mzazi wa Cassie.
Serikali ya Marekani ilikuwa imependekeza Combs ahukumiwe kifungo cha kati ya miezi 51 hadi 63, lakini upande wa utetezi uliomba kifungo kifupi cha kati ya miezi 21 hadi 27. Hatimaye, mahakama iliamua kumpa kifungo cha miezi 50, sambamba na adhabu ya kulipa faini na kipindi cha uangalizi baada ya kifungo.
Kwa hukumu hiyo, muda aliokaa mahabusu tangu kukamatwa kwake mwaka 2024 utahesabiwa katika kifungo chake cha sasa.




