Baada ya kushindwa kutokea uwanjani katika mechi ya Ligi ya Championship, Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi (Kamati ya TPLB) imeitoza Stand United ya Shinyanga faini ya Sh milioni 10 na kuamuru ilipe fidia ya maandalizi ya mchezo huo.
Aidha, Hausung FC ya Njombe imepewa ushindi wa mabao 3–0 na pointi tatu baada ya Stand United kushindwa kufika kwenye Uwanja wa Amani mkoani Njombe kwa ajili ya mchezo wa raundi ya nne wa ligi hiyo.
Uamuzi huo umetolewa katika kikao cha kamati hiyo kilichofanyika Novemba 11, 2025, kupitia mwenendo wa michezo mbalimbali ya Ligi Kuu Tanzania Bara na Championship.
Kwa mujibu wa taarifa ya Bodi ya Ligi, kamati pia imemfungia kwa mwaka mmoja Mwenyekiti wa Stand United, Stivian Antitius, kwa kosa la timu yake kushindwa kufika kituoni, kwa mujibu wa Kanuni ya 31:1 (1.1, 1.2, 1.3 & 1.4) ya Championship.
Kupitia ushindi huo wa chee, Hausung imepata pointi tatu zake za kwanza baada ya kupoteza michezo mitatu ya awali. Stand United, ambayo ilishuka daraja kutoka Ligi Kuu msimu wa 2020/2021, sasa haina pointi yoyote baada ya mechi nne.
Kamati hiyo pia imeipa onyo Stand United kwa kuchelewa kufika uwanjani katika mchezo dhidi ya Transit Camp, uliochezwa Oktoba 24, 2025 kwenye Uwanja wa Kituo cha Michezo cha TFF Kigamboni, Dar es Salaam, ambapo walifungwa 3–1.
Wakati huo huo, Songea United nayo imepewa onyo kali kwa kuchelewa kuwasili uwanjani katika mechi dhidi ya Transit Camp, iliyomalizika kwa kipigo cha 3–1, baada ya kuwasili saa 9:10 alasiri badala ya muda wa saa 8:30 uliowekwa na kanuni.




