VICTORIA FALLS, ZIMBABWE — Waziri wa Kilimo, Dkt. Daniel Chongolo, ameongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) unaowakutanisha mawaziri wanaosimamia sekta za kilimo, usalama wa chakula, mifugo, uvuvi na ufugaji wa viumbe maji.
Mkutano huo umefanyika Mei 29, 2026 mjini Victoria Falls, Zimbabwe, ukilenga kujadili mikakati ya kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika sekta hizo muhimu kwa maendeleo ya uchumi na ustawi wa wananchi wa nchi wanachama wa SADC.

Kabla ya mkutano wa mawaziri, kulifanyika kikao cha wataalamu tarehe 27 na 28 Mei 2026 ambapo wajumbe walijadili na kuandaa masuala mbalimbali ya kisekta kwa ajili ya kuwasilishwa katika ngazi ya mawaziri.
Katika mkutano huo, Dkt. Chongolo aliambatana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayeshughulikia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula, Profesa Peter Msoffe, ambaye pia aliongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano wa ngazi ya wataalamu.
Miongoni mwa ajenda zilizojadiliwa ni kuimarisha uzalishaji wa kilimo, usalama wa chakula, maendeleo ya mifugo, uvuvi na ufugaji wa viumbe maji, pamoja na kuimarisha ushirikiano wa nchi wanachama katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta ya kilimo katika ukanda wa SADC.
Dkt. Chongolo alipowasili nchini Zimbabwe alipokelewa na Balozi wa Tanzania nchini humo, Kamishna wa Polisi (CP) Suzan Kaganda.





