HomeBiasharaMalawi yaongoza nchi 10 zenye mafuta ghali zaidi Afrika; Tanzania haimo

Malawi yaongoza nchi 10 zenye mafuta ghali zaidi Afrika; Tanzania haimo

Wakati Watanzania wakiendelea kushuhudia kushuka kwa bei ya mafuta hadi Sh3,990 kwa lita ya petroli, orodha ya nchi 10 zenye mafuta ghali zaidi Afrika imeonyesha mabadiliko makubwa katika nafasi za bei, huku Tanzania ikiwa nje ya orodha hiyo kutokana na nafuu iliyopatikana.

Kwa mujibu wa takwimu zilizochapishwa na Business Insider Africa kupitia GlobalPetrolPrices, Malawi inaongoza kwa bei ya juu zaidi ya mafuta barani Afrika inayokadiriwa kufikia Sh10,000 kwa lita, ikifuatiwa na Rwanda (Sh5,400), Zimbabwe (Sh5,350), Jamhuri ya Afrika ya Kati (Sh5,000), Sierra Leone (Sh4,740), Ushelisheli (Sh4,520), Cape Verde (Sh4,460), Afrika Kusini (Sh4,350), Uganda (Sh4,320) na Kenya (Sh4,290).

Takwimu hizo zinaonyesha kuwa Tanzania imepiga hatua ya kupunguza gharama za mafuta kwa watumiaji wake, tofauti na baadhi ya nchi jirani na nyingine barani Afrika.

Mabadiliko haya yanatokana na tangazo la Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) EWURA la kushusha bei za mafuta kuanzia Julai 2026, hatua iliyotokana pia na kushuka kwa bei ya mafuta ghafi katika soko la dunia kufuatia kupungua kwa mvutano wa kisiasa Mashariki ya Kati.

Serikali kupitia sekta ya nishati imeeleza kuwa athari za kushuka kwa bei za dunia huchukua muda kabla ya kuonekana kwa watumiaji wa mwisho kutokana na mfumo wa uagizaji wa mafuta unaotumia muda wa awali wa manunuzi na usafirishaji.

Wachambuzi wa sekta ya nishati wanasema tofauti za bei za mafuta kati ya nchi hutokana na kodi na tozo, gharama za usafirishaji, uwezo wa kuhifadhi mafuta, thamani ya sarafu na sera za ruzuku za serikali mbalimbali.

Kwa Tanzania, kushuka kwa bei kunatarajiwa kusaidia kupunguza gharama za usafirishaji, uzalishaji na huduma, hatua inayoweza kuchangia kudhibiti mfumuko wa bei na kupunguza gharama za maisha iwapo mwenendo wa soko la dunia utaendelea kuwa tulivu.

Aidha, kutokuwamo kwa Tanzania katika orodha ya nchi 10 zenye mafuta ghali zaidi Afrika kunatafsiriwa kama ishara ya kuimarika kwa ushindani wa soko la ndani na kuanza kuonekana kwa manufaa kwa watumiaji wa kawaida.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments