HomeBiasharaTPSF yatetea PID Levy Sekta Viwanda

TPSF yatetea PID Levy Sekta Viwanda


Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) limesema utekelezaji wa Tozo ya Maendeleo ya Miundombinu ya Bandari (PID Levy), ulioanza rasmi Julai 1, 2026, utakuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya sekta ya viwanda na uchumi wa taifa kwa ujumla.

Kwa mujibu wa TPSF, mizigo inayolipa ushuru wa forodha itatozwa asilimia 4.5 ya ushuru huo, huku malighafi za viwandani na mizigo iliyosamehewa ushuru ikitozwa asilimia 1.5, hatua inayolenga kulinda viwanda vya ndani, kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika soko la ndani na la kimataifa.

Shirikisho hilo limesema limekuwa likishirikiana na Serikali katika kuhakikisha mfumo wa tozo hiyo unaleta uwiano kati ya uhitaji wa kuwekeza katika miundombinu ya bandari na kuimarisha mazingira rafiki ya biashara kwa sekta binafsi.

TPSF imefafanua kuwa PID Levy haitatozwa kwa mizigo ya kimiminika kwa wingi (Liquid Bulk Cargo), huku mizigo mingine ya uagizaji ikiendelea kutozwa kwa viwango vilivyowekwa na mamlaka husika.

Kwa mujibu wa shirikisho hilo, tofauti ya viwango vya asilimia 4.5 na 1.5 imewekwa makusudi ili kuhakikisha viwanda vya ndani havikabiliwi na ongezeko kubwa la gharama za uzalishaji, hususan kwa malighafi zinazotumika katika uzalishaji wa bidhaa mbalimbali.

TPSF imesisitiza kuwa malighafi na bidhaa zinazotumika katika viwanda ni msingi wa uzalishaji wa ndani, hivyo kupunguziwa tozo kutasaidia kuongeza uwekezaji mpya, kukuza ajira na kuinua tija ya viwanda nchini.

Aidha, shirikisho hilo limesema mapato yatakayokusanywa kupitia PID Levy yataelekezwa katika upanuzi na uboreshaji wa miundombinu ya bandari, kuongeza uwezo wa kupokea na kuhudumia mizigo, kupunguza msongamano wa meli na kuharakisha utoaji wa huduma bandarini.

TPSF imeeleza kuwa maboresho hayo yatawanufaisha wafanyabiashara moja kwa moja kupitia kupungua kwa gharama za usafirishaji na kuongeza ufanisi katika mnyororo mzima wa ugavi wa bidhaa.

Shirikisho hilo limeongeza kuwa bandari zenye miundombinu bora ni nguzo muhimu ya ukuaji wa uchumi, kwani huongeza kasi ya biashara, kuvutia uwekezaji na kuiwezesha Tanzania kuendelea kuwa lango kuu la biashara kwa nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini.

Aidha, TPSF imewahimiza wanachama wake na wadau wa sekta binafsi kuendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa PID Levy, ikisisitiza kuwa uwekezaji wa sasa katika miundombinu ya bandari ndio msingi wa uchumi imara na shindani kwa miaka ijayo.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments