Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limekabidhi magari tisa aina ya Toyota Hilux yenye thamani ya shilingi bilioni 1.6 pamoja na bajaji 28 zenye thamani milioni 291 ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango mkakati wa shirika wa kuboresha huduma kwa wananchi na kuimarisha utendaji wa mkongo wa taifa.
Akizungumza leo Aprili, 29 2026 jijini Dar es Salaam katika hafla ya makabidhiano hayo, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Moremi Marwa amesema kuwa ununuzi wa vitendea kazi hivyo unatokana na faida iliyopatikana ndani ya shirika, na kwamba hatua hiyo inalenga kuhakikisha huduma za mawasiliano zinaendelea kuboreka kwa kasi na ufanisi zaidi.




“Magari haya tisa aina ya Toyota Hilux yatasaidia shughuli za kuhudumia mkongo wa taifa. Mafundi wetu watakuwa na uwezo wa kufika haraka maeneo yenye changamoto kama kukatika kwa fiber au hitilafu nyingine ili kuhakikisha wateja wetu wanapata huduma bora wakati wote,” amesema.
Ameongeza kuwa bajaji 28 zilizonunuliwa zitasaidia kusogeza huduma za “fiber mlangoni kwako” kwa wananchi hasa katika maeneo ya mijini ambapo mahitaji ya huduma za intaneti yanaongezeka kwa kasi.
“Tunataka kuwafikia wateja wetu kwa karibu zaidi. Bajaji hizi zitasaidia mafundi na timu za biashara kufika kwa haraka maeneo yenye changamoto na kutoa huduma kwa ufanisi mkubwa,”ameeleza.
Mbali na magari hayo, TTCL pia imenunua magari ya biashara aina ya Hiace yatakayosaidia wafanyakazi wa shirika kuwafikia wateja wapya na kutoa huduma katika maeneo mbalimbali nchini bila changamoto za usafiri.
Amesema kuwa uwekezaji huo umetokana na mafanikio ya kifedha yaliyopatikana kupitia utekelezaji wa mpango mkakati wa shirika hilo ulioanza mwaka jana.
Aidha, TTCL imeendelea kutekeleza mradi wa “Fiber Mlangoni Kwako” katika mikoa mbalimbali nchini ikiwemo Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Iringa, Mbeya, Zanzibar na Arusha.




Amesema lengo la shirika ni kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanafikiwa na huduma za intaneti ya kasi kwa kujenga miundombinu kwanza kabla ya wateja kuomba huduma.
TTCL pia imeweka malengo ya kufikia maunganisho milioni moja ndani ya miaka mitatu ijayo kama sehemu ya kuendelea kupanua huduma za mawasiliano nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Mhandisi Cecil Francis, amesema kuwa ununuzi wa vitendea kazi vipya ni sehemu ya jitihada za shirika kuhakikisha huduma za mawasiliano zinaendelea kuboreshwa kwa wananchi kote nchini.
Amesema licha ya changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya mawasiliano duniani, TTCL imeendelea kuwekeza katika miundombinu na vifaa vya kisasa ili kuwahudumia wateja wake kwa ufanisi zaidi, hususan wanaotumia huduma za mkongo wa taifa na huduma za “Fiber Mlangoni Kwako”.
Ameeleza kuwa kwa niaba ya wafanyakazi wa TTCL, wanaahidi kutumia vifaa hivyo kwa weledi mkubwa ili kuhakikisha changamoto za mawasiliano zinatatuliwa kwa haraka na huduma zinaendelea kuwa bora zaidi.






