Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhandisi Hamad Yussuf Masauni ameshiriki Kikao kilichowakutanisha viongozi kutoka mataifa mbalimbali ikiwa ni juhudi za kupambana na kuenea kwa hali ya Jangwa na Ukame katika eneo la kuboresha afya ya Udongo na matumizi sahihi mbolea.
Kikao hicho kilifanyika katika Ubalozi wa Uingereza nchini Mongolia Agosti 26, 2026 katika jijini Ulaanbaatar kiliwakutanisha Mwakilishi Maalumu wa Uingereza nchini Mongolia Ruth Davis, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Beth Bechdol, Moses Vilakati, Kamishna wa Umoja wa Afrika (AU) anayeshughulikia Kilimo, Maendeleo ya Vijijini, Uchumi wa Buluu na Mazingira Endelevu pamoja na viongozi wengine kutoka Mataifa mbalimbali.
Amesema Tanzania inakuza malisho endelevu, mipango shirikishi ya matumizi ya ardhi, urejeshaji wa maeneo ya malisho, miundombinu iliyoboreshwa ya maji, mifumo ya tahadhari ya mapema ya ukame na uzalishaji bora wa mifugo.
“Tunatoa wito na elimu juu ya hali ya hewa, maendeleo na uwekezaji binafsi na ushirikiano kwa umma na binafsi ili kuongeza urejeshaji wa maeneo ya malisho ili kila mmoja awe na wajibu wa kulinda udongo.”




“Kwa Tanzania, maeneo ya malisho ni muhimu sana kwa uzalishaji wa mifugo, usalama wa chakula, bayoanuwai, rasilimali za maji na maisha ya watu vijijini. Kutokana na idadi ya watu inayokadiriwa kufikia milioni 61.7, kuna ongezeko la shinikizo kwenye ardhi, maji na rasilimali asili.
Ameongeza kuwa, kwa mujibu wa Ripoti ya Utafiti wa Sampuli ya Kilimo wa Mwaka 2022/23 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Tanzania ilikuwa na kaya za wakulima zipatazo milioni 8.97, ambapo asilimia 60.6 kati ya hizo zilijishughulisha na ufugaji. Hii inadhihirisha umuhimu wa maeneo bora ya malisho kwa jamii na uchumi.
Hata hivyo, maeneo ya malisho yanakabiliwa na shinikizo linaloongezeka kutokana na ukame, uharibifu wa ardhi, ufugaji kupita kiasi, mabadiliko ya matumizi ya ardhi, uhaba wa maji, uchomaji misitu na mabadiliko ya hali ya hewa.




Amesema kwa kutambua hilo Tanzania imejiwekea mikakati kupitia Programu ya Kitaifa ya Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame (2025 – 2030), unaozingatia utayari wa ukame, tahadhari ya mapema na usimamizi endelevu wa ardhi.
Mhe. Masauni amesema jitihada hizi zinaendana Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 hasa Nguzo ya Tatu ya Uhifadhi wa Mazingira na Ustahimilivu wa Mabadiliko ya Tabianchi, inayounganisha urejeshaji wa maeneo ya malisho na mabadiliko ya mifugo, usalama wa chakula na ustahimilivu wa hali ya hewa.
Waziri Masauni yupo nchini Mongolia kushiriki Mkutano wa Kumi na Saba wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame (UNCCD COP 17) ulionza tangu Agosti 24, 2026.







