Tuesday, March 17, 2026
spot_img
HomeHabariVAT kuondolewa kusaidia wananchi nishati safi

VAT kuondolewa kusaidia wananchi nishati safi

Serikali imeondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye uagizaji wa mitungi ya gesi (LPG), mitungi mikubwa ya gesi pamoja na vifaa vya kuzalisha mkaa mbadala (carbonizers), ikiwa ni hatua ya kupunguza gharama na kurahisisha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kwa wananchi.

Akizungumza Machi 17, 2026 wilayani Morogoro wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Nishati Safi ya Kupikia, Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amesema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala na kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa.

Amesema Serikali chini ya Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan, imeweka kipaumbele katika kuhakikisha wananchi wanapata nishati safi ya kupikia kupitia upatikanaji wa mitungi ya gesi, majiko banifu, gesi vunde na upanuzi wa umeme hadi ngazi ya vitongoji. Ameongeza kuwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kupitia kampuni ya MECS tayari limewezesha wateja 480 kupata majiko ya umeme kwa mfumo wa kulipa kidogokidogo kupitia bili za umeme.

Waziri Ndejembi amesema Serikali inalenga kufikia asilimia 75 ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2030 na asilimia 80 ifikapo 2034. Amefafanua kuwa mafanikio tayari yanaonekana kwani watumiaji wameongezeka kutoka asilimia 6 mwaka 2024 hadi kufikia asilimia 23.2 kwa sasa.

Amesisitiza umuhimu wa wadau kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili kubadili mitazamo hasi kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia, pamoja na kuongeza ubunifu na kupanua miundombinu ya usambazaji wake. Amebainisha kuwa zaidi ya asilimia 50 ya kaya nchini bado zinategemea kuni na mkaa.

Aidha, ametoa wito kwa wadau kutumia kongamano hilo kama jukwaa la kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na asasi za kiraia ili kuongeza upatikanaji wa nishati safi, ambayo ni muhimu kwa afya, mazingira, uchumi na usawa wa kijinsia.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, amesema ajenda ya nishati safi ya kupikia ni muhimu kwa maendeleo endelevu na amewahimiza wananchi kuunga mkono jitihada za Serikali. Pia ameishauri Wizara ya Nishati kushirikiana na taasisi za fedha kuwawezesha wajasiriamali kutumia pumba za mpunga kuzalisha mkaa mbadala kutokana na upatikanaji wake kwa wingi mkoani humo.

Naye Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati (Umeme na Nishati Jadidifu), Nolasco Mlay, amesema kongamano hilo limewakutanisha wadau mbalimbali kutoka sekta za umma, binafsi na mashirika ya kimataifa ili kubadilishana uzoefu na kujadili mikakati ya kuendeleza matumizi ya nishati safi nchini.

Awali, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi,Kadari Singo, amesema lengo la kongamano hilo ni kuongeza uelewa wa manufaa ya nishati safi ya kupikia pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya wadau, huku pia likiwa jukwaa la kujadili changamoto, suluhisho na fursa zilizopo katika sekta hiyo.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments