Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Hamis Livembe, amesema wafanyabiashara wamefurahishwa na ripoti ya Tume ya Rais ya Kutathmini Maboresho ya Mifumo ya Kodi nchini kwa kuwa imeakisi maoni na mapendekezo yao.
Amesema awali kulikuwa na mashaka kuhusu uundwaji wa tume hiyo, hasa kutokana na kukosekana kwa uwakilishi wa wafanyabiashara na kuwepo kwa maofisa wa Serikali pekee. Hata hivyo, ripoti iliyowasilishwa imeondoa hofu hiyo baada ya kugusa changamoto zilizokuwa zikilalamikiwa.
Livembe alitoa kauli hiyo Machi 19, 2026 akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara, kufuatia tume hiyo iliyoongozwa na Balozi Ombeni Sefue kukabidhi ripoti yake kwa Rais wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan, Machi 18 mwaka huu.
“Hoja zetu zimesikilizwa na zimeonekana za msingi. Kwa sasa tunasubiri kuona utekelezaji wake na namna ambavyo mapendekezo hayo yatavyoboresha mazingira ya biashara,” amesema Livembe.
Aidha, ameeleza kuwa ingawa awali tume hiyo ilikosa imani kutokana na muundo wake, mapendekezo yaliyotolewa yamejibu kilio cha wafanyabiashara na kurejesha imani kwa wadau.
Ameipongeza tume hiyo kwa usikivu wake na kwa kuja na mapendekezo yaliyogusa kwa kina changamoto zote zilizokuwa zikikabili sekta ya biashara nchini.




