Kocha maarufu wa soka, Jürgen Klopp, amekanusha vikali taarifa zinazomuhusisha na kujiunga na Real Madrid, akizitaja kuwa hazina ukweli wowote.
Akizungumza kuhusu uvumi huo, Klopp amesema hajawahi kuwasiliana na klabu hiyo, wala wakala wake hajapokea mawasiliano yoyote kutoka kwa mabingwa hao wa Hispania. Kauli hiyo imekuja kufuatia taarifa zilizokuwa zikienea mitandaoni zikimhusisha na uwezekano wa kuinoa miamba hiyo ya La Liga.
“Real Madrid hawajanipigia simu hata mara moja. Hizi ni stori za magazeti tu, na zinakera,” amesema Klopp.
Mbali na hilo, Klopp pia alizungumzia uvumi uliokuwa ukimhusisha na Atlético Madrid, akieleza kwa utani kuwa klabu hizo zinapaswa kwanza kuwasiliana naye kabla ya jina lake kuhusishwa nazo.
Kauli hizi zinaweka bayana kuwa hadi sasa hakuna mawasiliano rasmi kati ya Klopp na klabu yoyote ya Hispania, licha ya uvumi unaoendelea kusambaa, huku kocha huyo akiendelea kubaki kimya kuhusu hatma yake ya baadaye kisoka.




