Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), William Lukuvi, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 70.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi, Lukuvi amefariki saa 1:00 asubuhi ya Jumatano, Machi 25, 2026 katika Hospitali ya Benjamin Mkapa alipokuwa akipatiwa matibabu jijini Dodoma.
Kifo hicho kimetangazwa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kupitia taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Moses Kusiluka.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa kiongozi huyo alifariki dunia kutokana na ugonjwa wa mshtuko wa moyo. Rais Samia ametuma salamu za rambirambi kwa Spika wa Bunge, familia ya marehemu, wananchi wa Jimbo la Isimani mkoani Iringa, pamoja na Watanzania wote.
Hayati Lukuvi pia alikuwa Mbunge wa Jimbo la Isimani tangu mwaka 1995, akihudumu kwa zaidi ya miaka 30, na alikuwa miongoni mwa wabunge waandamizi waliotoa mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa.




