Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Victoria Mwanziva, ameshiriki kikamilifu na Kamati ya Maafa ya Halmashauri ya Wilaya ya Mtama katika zoezi la utoaji wa misaada ya kibinadamu kwa waathirika wa mafuriko, lengo likiwa ni kuwafariji na kuwasaidia kurejea katika hali yao ya kawaida.
Mafuriko hayo yaliripotiwa kutokea Machi, 2026 katika kijiji cha Namunda, Kitongoji cha Nusura, ambapo yalisababisha kusimama kwa shughuli za maendeleo kwa takribani saa nne na nusu, ikiwemo shughuli za usafirishaji.
Kutokana na athari hizo, jumla ya kaya 61 zenye watu 164 ziliathirika, huku baadhi yao wakikosa makazi na mali muhimu. Hali hiyo ililazimu mamlaka husika kuchukua hatua za haraka za kuwasaidia waathirika.





Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kutembelea wahanga, kuwapatia hifadhi ya muda, pamoja na kutoa elimu ya kujikinga na magonjwa ya mlipuko yanayoweza kusababishwa na mafuriko.
Vifaa vilivyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu ni pamoja na magodoro 138, blanketi 138, mahema makubwa matano yenye uwezo wa kuhifadhi zaidi ya watu 20 kila moja, boksi 10 za sabuni, pamoja na ndoo 100 kwa ajili ya kunawa mikono na kuimarisha usafi.
Akizungumza katika zoezi hilo, Mwanziva ameitaka Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtama kwa kushirikiana na Mratibu wa Kamati ya Maafa, Ndg. Ismail Mbani, kufanya tathmini ya haraka ya athari za mafuriko kwenye mashamba ya wananchi.
Amesisitiza umuhimu wa kupata takwimu sahihi za ukubwa wa mashamba yaliyoathirika na mahitaji halisi, ili kuwezesha hatua za haraka za msaada, akibainisha kuwa taarifa hizo zitasaidia kufanikisha mawasiliano na wadau kwa ajili ya msaada zaidi.





