Mjumbe wa Tume ya Kuchunguza matukio ya wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, Balozi Paul Mella, amesema vyombo vya ulinzi na usalama vilizidiwa na kasi ya matukio ya ghasia yaliyotokea, huku mipango mingi ya matukio hayo ikipangwa mtandaoni.
Amesema tofauti na miaka ya nyuma ambapo mipango ya matukio kama hayo ilifanyika kwa njia za ana kwa ana, sasa teknolojia imebadilisha hali hiyo na kuruhusu mipango kufanyika mtandaoni bila wahusika kuonekana kirahisi.
“Miaka ya nyuma ilikuwa ukitaka kupanga mambo kama haya unapanga ardhini kisha unakuja field, lakini kutokana na teknolojia sasa hivi mambo yanapangwa kwenye mtandao, humuoni mtu anayepanga na wanaweza wakapanga wakafanikisha wakawa wako mbele kuliko wale wanaozuia,” amesema Mella akizungumza na wanahabari Aprili 28, 2026 jijini Dar es Salaam.
Amesema uchunguzi wa Tume umebaini kuwa teknolojia ya sasa inawawezesha watu kupanga matukio kwa njia ya mtandao, ambapo ushahidi unaonyesha kuwa taarifa zilikuwepo mtandaoni kabla ya matukio kutokea, huku pia kukiwa na watu wachache waliokuwa wakiratibu shughuli hizo kwa njia za kawaida ardhini.
Kwa mujibu wake, Tume ilitembelea magereza mbalimbali yaliyokuwa na watuhumiwa na kupata fursa ya kuzungumza nao pamoja na waathirika waliowasilisha ushahidi, ikiwemo picha na taarifa nyingine muhimu.
“Tuliwafikia baadhi ya watuhumiwa wanaoonekana kwenye CCTV, walitueleza mengi na kukiri kuwa walifuata mkumbo,” ameongeza.
Aidha, amesema vyombo vya ulinzi vilipata taarifa hizo, lakini vilizidiwa na kasi ya matukio hayo, hali inayohusishwa na kile kinachojulikana kitaalamu kama “intelligence lapse,” yaani upungufu wa taarifa kamili au uchambuzi wake.
Amefafanua kuwa mbinu zilizotumika hazikuwa za kawaida, kwani vyombo vya ulinzi vilitegemea maandamano ya mkusanyiko kutoka eneo moja kwenda eneo jingine, lakini badala yake kulikuwa na matukio yaliyotawanyika katika maeneo mengi kwa wakati mmoja, jambo lililofanya udhibiti kuwa mgumu.




