Mbunge wa Tunduru Kaskazini, Ado Shaibu Ado, amesema kuna mapungufu katika mchakato wa bajeti unaoendelea katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akidai sekta ya kilimo na mchakato wa Katiba mpya havijapewa uzito unaostahili.
Akizungumza na waandishi wa habari, Shaibu amesema kupitishwa kwa bajeti bila upinzani mkubwa si kigezo cha ubora wake, bali kunatokana na wabunge wa upinzani kukosa nafasi ya kutosha kuwasilisha hoja zao kwa kina.
Ameeleza kuwa muda mfupi wa kuchangia mijadala umekuwa ukilazimisha wabunge kutoa hoja kwa ufupi, jambo linalowanyima wananchi uelewa wa kina kuhusu masuala yanayojadiliwa bungeni.
Kutokana na changamoto hiyo, amesema wameamua kutumia vyombo vya habari kufikisha ujumbe wao kwa wananchi.
Kuhusu Katiba mpya, Shaibu amesema bado haijapewa kipaumbele kinachostahili licha ya umuhimu wake kwa mustakabali wa taifa. Aidha, amesisitiza kuwa sekta ya kilimo, inayogusa maisha ya Watanzania wengi, inapaswa kupewa nafasi kubwa zaidi katika bajeti.
Pia ameitaka Serikali kusimamia kwa karibu utekelezaji wa bajeti na mipango ya maendeleo, akionya kuwa kupuuzwa kwa sekta muhimu kama kilimo kunaweza kuathiri ustawi wa wananchi.




