Katika maadhimisho ya miaka 50 ya Tanzania Bureau of Standards (TBS), mwakilishi wa SICPA Tanzania, Bw. Alfred Mapunda, amesema mafanikio ya Tanzania katika kujenga uchumi wa kisasa yanategemea uaminifu wa wananchi kwa bidhaa, huduma na mifumo inayosimamia ubora wake.
Mapunda alisema kwa nusu karne iliyopita, TBS imeendelea kuwa nguzo muhimu katika kuhakikisha viwango, ubora na usalama wa bidhaa vinazingatiwa, hatua iliyochangia kujenga mazingira bora ya biashara na kulinda maslahi ya walaji.
Alieleza kuwa ushirikiano kati ya TBS, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), vyombo vya utekelezaji wa sheria na SICPA kupitia Mfumo wa Kitaifa wa Uwekaji Alama kwenye Mafuta umeleta mafanikio makubwa, ikiwemo kuimarika kwa ubora wa mafuta, kuongezeka kwa uwazi wa soko, ushindani wa haki na ukusanyaji wa mapato ya serikali.
Kwa mujibu wake, mafanikio hayo yanaonyesha umuhimu wa ushirikiano wa taasisi mbalimbali katika kujenga mifumo madhubuti inayolinda walaji, kusaidia wafanyabiashara wanaozingatia sheria na kuongeza imani ya wananchi kwa taasisi za umma.

“Miaka 50 iliyopita, uamuzi ulifanywa kwamba ubora usiwe wa kubahatisha bali uwe msingi wa maendeleo ya taifa. Leo tunasherehekea matokeo ya uamuzi huo na mchango wa TBS katika kujenga Tanzania yenye viwango imara, uaminifu na maendeleo endelevu,” alisema Mapunda.







