Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeufungia Uwanja wa CCM Liti (Singida) na Uwanja wa Sokoine (Mbeya) kutokana na kukosa vigezo vya kikanuni.
Ofisa Habari wa TFF, Clifford Ndimbo, amesema timu zinazotumia viwanja hivyo zitalazimika kutafuta uwanja mwingine hadi zitakapokamilisha marekebisho.
Uwanja wa Sokoine unatumika na Mbeya City na Tanzania Prisons, huku KenGold ikiruhusiwa kuutumia kwa mchezo mmoja pekee kabla ya marufuku kuanza.

Meneja wa uwanja huo, Modestus Mwaluka, amesema kasoro zilizojitokeza zilisababishwa na gwaride la halaiki lililoharibu nyasi, lakini marekebisho yameanza mara moja.
“Ndani ya siku nne kila kitu kitakuwa sawa,” alisema Mwaluka.
Hata hivyo, Mbeya City haitapata athari wiki hii kwani inacheza ugenini dhidi ya KMC jijini Dar es Salaam.




