HomeHabariBonde la Wami Ruvu wapanda miti 500 kulinda Mto Mpiji

Bonde la Wami Ruvu wapanda miti 500 kulinda Mto Mpiji

BAGAMOYO —Wananchi, viongozi wa serikali na wadau wa mazingira wameungana katika hafla ya upandaji miti kando ya Mto Mpiji, katika Kitongoji cha Kimere, Kata ya Mapinga, Wilaya ya Bagamoyo, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Mazingira.

Zoezi hilo limeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Bodi ya Maji ya Bonde la Wami-Ruvu na vikundi vya usafishaji wa mito, ambapo miti 500 imepandwa katika hifadhi ya Mto Mpiji unaotenganisha Mkoa wa Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani.

Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Bagamoyo, Stella Msofe, amesema miti iliyopandwa inapaswa kutunzwa ili iweze kuleta manufaa yaliyokusudiwa, ikiwemo kuboresha mazingira na kuchangia maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi.

Amesema wananchi wanapaswa kuheshimu mipaka iliyowekwa katika maeneo ya hifadhi na kuacha kufanya shughuli za kibinadamu zinazoweza kusababisha uharibifu wa mazingira.

“Sisi kama Wilaya ya Bagamoyo tunapaswa kuhakikisha tunaepuka shughuli za kibinadamu katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya hifadhi ili kulinda vyanzo vya maji na mazingira yetu,” amesema Msofe.

Aidha, amesema kuwa katika kuadhimisha Wiki ya Mazingira, wakazi wa Bagamoyo wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kulinda mazingira na kudumisha usafi wa maeneo yao, hasa ikizingatiwa kuwa Bagamoyo ni lango muhimu la biashara na utalii.

Zoezi hilo pia liliambatana na uzinduzi wa alama maalum zinazoonyesha mipaka kati ya hifadhi ya Mto Mpiji na maeneo ya makazi ya watu.

Maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo: “Dira 2050: Tuwajibike Kukijani Tanzania.”

Kwa upande wake, Mkuu wa Ofisi ya Wami-Ruvu Dar es Salaam kutoka Bodi ya Maji ya Bonde la Wami-Ruvu, Diana Kimpute, amesema upandaji wa miti katika eneo la Kimere unalenga kulinda na kuhifadhi vyanzo vya maji vya Mto Mpiji.

“Tumekuja kupanda miti kwa ajili ya kutunza vyanzo vya maji. Tunawaomba wananchi watupe ushirikiano katika kuitunza miti hii na kulinda vyanzo vya maji,” amesema Kimpute.

Ameongeza kuwa wananchi wanapaswa kuepuka kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60 kutoka ukingo wa mto, kwa mujibu wa sheria na miongozo ya uhifadhi wa mazingira.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Usafishaji Mito na Mazingira, Jacob Eliasa, amesema shughuli hiyo ni ishara ya dhamira ya wananchi katika kuhifadhi mazingira na mito kwa ajili ya kujenga Tanzania ya kijani.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kimere, Pazi Urembo, amesema Mto Mpiji umekuwa ukisababisha changamoto mbalimbali wakati wa msimu wa mvua, hivyo upandaji wa miti utasaidia kupunguza athari hizo na kuimarisha uhifadhi wa mazingira.

Amesema viongozi wa kijiji na wananchi wataendelea kufuatilia na kutunza miti hiyo ili kuhakikisha inakua na kufikia malengo yaliyokusudiwa.

“Miti 500 bado haitoshi kulingana na mahitaji ya mazingira yetu. Tunaendelea kusubiri miche mingine na tutaongeza ulinzi ili kuhakikisha hakuna anayeharibu miti au kufanya uchimbaji holela katika eneo la mto,” amesema Urembo.

Amesisitiza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watu watakaobainika kujihusisha na uchimbaji holela au shughuli nyingine zinazoharibu mazingira ya mto.

Mkazi wa Kizimkazi, Paulina George, amesema wananchi wana wajibu wa kuitunza miti hiyo kwa kuwa inaleta manufaa makubwa kwa afya, mazingira na maendeleo ya jamii.

Wananchi wamehimizwa kuendelea kuitunza miti iliyopandwa ili waweze kunufaika na mazingira bora pamoja na fursa mbalimbali za kiuchumi zitakazotokana na uwepo wa miti hiyo.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments