Wednesday, April 29, 2026
spot_img
HomeHabariExim, Serikali kuimarisha ufadhili elimu

Exim, Serikali kuimarisha ufadhili elimu

Serikali imeendelea kupanua fursa za elimu ya juu kwa vijana, baada ya kuanza mazungumzo na sekta binafsi ili kuongeza ufadhili katika taaluma za kisasa zinazohitajika zaidi kwenye soko la ajira.

Katika hatua hiyo, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imekutana na timu ya Benki ya Exim kujadili namna ya kuimarisha ushirikiano katika kuendeleza elimu nchini, hususan kwa wanafunzi wa elimu ya juu.

Timu ya Benki ya Exim iliyoongozwa na Afisa Mkuu wa Fedha, Shani Kinswaga, pamoja na viongozi wengine waandamizi, ilifanya mazungumzo na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, jijini Dodoma Aprili 27, 2026.

Mazungumzo hayo yalilenga kuangazia fursa za ufadhili kwa wanafunzi wanaosomea masomo ya kimkakati kama sayansi ya data (Data Science), akili unde (Artificial Intelligence) na sayansi shirikishi, ambayo yanaendelea kuwa na umuhimu mkubwa katika dunia ya sasa ya teknolojia.

Pia, pande hizo mbili zilijadili uwezekano wa kupanua wigo wa ushirikiano katika kusaidia maendeleo ya elimu kwa ujumla, ikiwemo kuongeza uwekezaji katika rasilimali watu wenye ujuzi wa kisasa.

Hatua hiyo inaelezwa kuwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha vijana wanapata elimu inayokidhi mahitaji ya soko la ajira na kuwawezesha kushindana kimataifa.

Kwa ujumla, ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za kifedha unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa ufadhili wa masomo na kuchochea maendeleo ya sekta ya elimu nchini.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments