Tuesday, April 28, 2026
spot_img
HomeBiasharaSGR yapata fedha Sh. trilioni 3.4

SGR yapata fedha Sh. trilioni 3.4

Wizara ya Uchukuzi imesaini mkataba wa dola za Marekani bilioni 1.277 (sawa na takribani trilioni 3.4) kwa ajili ya ujenzi wa vipande viwili vya Reli ya Kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR), hatua inayotarajiwa kuimarisha usafiri na kuchochea uchumi wa wananchi.

Mkataba huo unahusisha ujenzi wa kipande cha Makutupora hadi Isaka chenye urefu wa kilometa 368 pamoja na Tabora hadi Isaka kilometa 165, na kufanya jumla ya kilometa 533. Utiaji saini umefanyika Aprili 28, 2026 jijini Dodoma ukihudhuriwa na viongozi wa serikali, taasisi za kifedha na wadau wa maendeleo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Fedha, Balozi Dk. Khamis Mussa Omar, amesema ufadhili huo umetolewa na mashirika matatu ya fedha kutoka Italia, Sweden na Poland, ili kuharakisha utekelezaji wa mradi huo muhimu wa kimkakati.

Amesema maendeleo ya ujenzi wa SGR yanaendelea vizuri, ambapo kipande cha Dar es Salaam hadi Dodoma tayari kimekamilika na kuanza kutoa huduma, huku sehemu nyingine zikiendelea kujengwa, hatua inayolenga kuunganisha mtandao wa reli kwa zaidi ya kilometa 2,100 nchini.

Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema mradi huo ni wa kihistoria na utabadilisha Tanzania kuwa kitovu cha usafirishaji na usambazaji wa mizigo katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Ameeleza kuwa tangu kuanza kwa mradi huo mwaka 2017, tayari umeleta manufaa kwa wananchi ikiwemo kupunguza muda wa safari, gharama za usafiri na kiwango cha uchafuzi wa mazingira, pamoja na kutoa ajira kwa maelfu ya Watanzania.

Aidha, mradi huo unatarajiwa kufungua fursa mpya za biashara, uwekezaji na ajira, huku ukiunganisha mikoa mbalimbali na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa ndani na nje ya nchi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Natu Mwamba, ameishukuru jumuiya ya wadau wa maendeleo kwa ushirikiano wao, huku wakiahidi kuendelea kuisaidia Tanzania katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo inayolenga kuinua maisha ya wananchi.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments