Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Tumaini Nyamhokya, amewataka waajiri nchini kutekeleza amri ya Serikali ya kuongeza kima cha chini cha mishahara kwa wafanyakazi wa sekta binafsi.
Nyamhokya ametoa wito huo leo, alipotembelea banda la Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano katika maonesho ya Wiki ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi yanayoendelea mkoani Njombe.
Amesema Serikali ilitangaza kima hicho kipya cha chini cha mishahara ambacho kilianza kutumika Januari mwaka huu, lakini hadi sasa utekelezaji wake bado haujafikia kiwango kinachotarajiwa.

Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, ni takribani asilimia 80 ya waajiri katika sekta binafsi ndio wameanza kutekeleza agizo hilo.
“Nitoe wito kwa waajiri wote wa sekta binafsi nchini kuhakikisha wanatekeleza amri hii ya Serikali kwa kuongeza mishahara husika, hatua itakayochangia ustawi na kuongeza morali ya wafanyakazi,” amesema Nyamhokya.
Akiwa katika banda hilo, Nyamhokya amepokea maelezo kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa, ikiwemo elimu ya ajira, kinga ya jamii, sheria za kazi pamoja na mahusiano kati ya Serikali na makundi ya kijamii, yakiwemo taasisi za dini, mashirika yasiyo ya kiserikali na asasi za kiraia.
Amepongeza juhudi za maafisa wa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kutoa elimu kwa umma kupitia maonesho hayo, akisema hatua hiyo inaongeza uelewa wa wananchi kuhusu huduma na haki zao kazini.
Aidha, amewahamasisha wananchi na wafanyakazi kutembelea banda hilo ili kujifunza zaidi masuala ya ajira na kinga ya jamii.
Katika hatua nyingine, Nyamhokya amewasihi wafanyakazi wa mkoa wa Njombe na mikoa jirani kujitokeza kwa wingi kushiriki sherehe za Mei Mosi zinazotarajiwa kufanyika kitaifa mkoani humo.





