Zaidi ya wananchi 821 wa Kijiji cha Kigoda na sehemu ya Ndwati katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha wanatarajiwa kuondokana na adha ya maji baada ya kukamilika kwa mradi wa maji unaosogeza huduma hiyo karibu na makazi yao.
Awali, wananchi walilazimika kutembea umbali wa kilometa 2.5 kutafuta maji kutoka vyanzo visivyo salama, lakini sasa huduma hiyo itapatikana ndani ya umbali wa mita 400 na muda usiozidi nusu saa.
Akitoa taarifa leo Aprili 20 kwa kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Mwang’onda, Meneja wa RUWASA, Mhandisi Debora Kanyika, amesema mradi huo utasaidia kuinua uchumi wa wananchi kwa kuwaokoa muda waliokuwa wakitumia kutafuta maji.

Amebainisha kuwa mradi huo wenye thamani ya sh. milioni 546.7 unahusisha ujenzi wa tenki la maji la lita 100,000, vituo tisa vya kuchotea maji, mabwawa mawili ya kunyweshea mifugo, mfumo wa nishati ya jua na ulazaji wa mabomba ya kilometa 13.5.
Mradi huo ulianza Januari 8, 2024 kupitia mkandarasi LUKEDAN Company Limited na unatarajiwa kukamilika Juni 30 mwaka huu, ukiwa umefikia asilimia 90 ya utekelezaji.
Aidha, utekelezaji wake umechangia kutoa ajira 58 kwa wananchi, wengi wao wakiwa vijana, huku ukitarajiwa kuongeza upatikanaji wa maji wilayani humo kutoka asilimia 86.5 hadi 87.5.
Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson John, amesema Mwenge wa Uhuru unapitia miradi 26 yenye thamani ya sh. bilioni 162 inayolenga kuboresha huduma za kijamii na kuharakisha maendeleo ya wananchi.





