Friday, December 5, 2025
spot_img
HomeHabariWaratibu wa ICGLR wakutana Kinshasa kuandaa mkutano wa Mawaziri na Wakuu wa...

Waratibu wa ICGLR wakutana Kinshasa kuandaa mkutano wa Mawaziri na Wakuu wa Nchi

Kinshasa, DRC – Mkutano wa 20 wa Kawaida wa Waratibu wa Kitaifa wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) umefanyika leo, Novemba 10, 2025, jijini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Mkutano huo ni sehemu ya maandalizi ya Mkutano wa 19 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje (RIMC) na Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali (SUMMIT) wa Jumuiya hiyo, unaotarajiwa kufanyika Novemba 13 na 15, 2025, mtawalia.

Akifungua mkutano huo, Waziri wa Ushirikiano wa Kikanda wa DRC, Floribert Anzuluni Isiloketshi, amewasihi waratibu wa kitaifa kutumia kikao hicho kuandaa mapendekezo yatakayoboresha utendaji wa Sekretarieti ya Maziwa Makuu, ili iweze kutekeleza kwa ufanisi majukumu yake ya msingi, hususan katika kuimarisha amani, usalama na maendeleo katika nchi 12 wanachama wa ICGLR.

Tanzania, ambayo ni miongoni mwa waasisi wa ICGLR, inashiriki kikamilifu katika mkutano huo kupitia ujumbe unaoongozwa na Mratibu wa Kitaifa na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Afrika kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Ellen Maduhu.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa ICGLR, Balozi João Samuel Caholo, amesema licha ya mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wake, bado kuna haja ya kuongeza jitihada kuhakikisha amani ya kudumu na usalama vinapatikana katika Ukanda huo, hususan katika nchi za DRC, Jamhuri ya Sudan, Sudan Kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Balozi Caholo ameongeza kuwa umasikini, ukosefu wa usawa na wananchi kushindwa kunufaika na rasilimali za nchi zao ni miongoni mwa vyanzo vya migogoro barani Afrika, hivyo akatoa wito kwa viongozi kushughulikia chanzo cha migogoro hiyo ili kudumisha utulivu na maendeleo endelevu.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments