Monday, March 9, 2026
spot_img
HomeHabariNdejembi asisitiza ushirikiano utekelezaji miradi yenye kipaumbele kwa wananchi

Ndejembi asisitiza ushirikiano utekelezaji miradi yenye kipaumbele kwa wananchi

šŸ“ŒAhimiza kufanya kazi kwa kushirikiana na Wadau

šŸ“ŒAhimiza kufanyika kwa tafiti mbalimbali hasa katika gesi na mafuta

šŸ“ŒAkutana na Taasisi za PURA na TPDC

Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi ametoa wito kwa viongozi na watendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) pamoja na Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) kuimarisha ushirikiano katika kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati inayohusiana moja kwa moja na ustawi wa wananchi.

Akizungumza Novemba 24, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya kikazi iliyoangazia mazungumzo na uongozi wa bodi na menejimenti za taasisi hizo, Mhe. Ndejembi alisema Serikali inategemea utendaji wenye weledi, uwajibikaji na uwazi kutoka TPDC na PURA ili miradi ya kipaumbele itekelezwe kwa wakati na kwa viwango vya kimataifa.

ā€œNamshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniamini na kunipa nafasi hii. Nimeona ni vyema kukutana nanyi kwa lengo la kufahamiana, kujifunza na kuhakikisha tunaweka mikakati madhubuti ya kutekeleza majukumu yetu kwa kasi na bidii zaidi ili kuongeza upatikanaji wa nishati ya uhakika nchini,ā€ amesema Ndejembi.

Waziri huyo pia aliwataka viongozi wa taasisi hizo kupitia changamoto zinazoathiri kasi ya utekelezaji wa miradi na kuwasilisha mapendekezo ya maboresho yatakayoongeza tija.

Amesisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa ufanisi hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali imewekeza nguvu kubwa katika kuboresha miundombinu ya nishati na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje.

Aidha, aliwahimiza kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kufanya tafiti za kina kuhusu mafuta na gesi, akibainisha kuwa sekta hiyo ina ushindani mkubwa duniani hivyo inahitaji uongozi thabiti, mipango madhubuti na matumizi bora ya rasilimali ili kuhakikisha Tanzania inanufaika ipasavyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mussa Makame, alimshukuru Waziri kwa ziara hiyo na kuahidi kuboresha mifumo ya utendaji pamoja na kuimarisha ushirikiano baina ya taasisi kwa maslahi mapana ya Taifa. Alisema TPDC itaendelea kushirikiana na wadau wote muhimu ili kufanikisha malengo ya kitaifa.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Mhandisi Charles Sangweni, alieleza kuwa mamlaka hiyo inaendelea kuanzisha vyanzo vipya vya mapato na kuboresha usimamizi wa miradi ya mafuta na gesi. Aliahidi kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na kuongeza uwazi katika utoaji wa taarifa ili wananchi wapate ufahamu sahihi juu ya maendeleo ya miradi ya nishati nchini.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments