Serikali imetenga zaidi ya Shilingi bilioni 3.5 kwa ajili ya kuboresha meli ya MV Songea inayofanya safari zake kati ya bandari ya Kiwira mkoani Mbeya na bandari ya Mbamba Bay, mkoani Ruvuma kupitia Ziwa Nyasa.
Hayo yamebainishwa na Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO), Abdulrahman Salim, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika maonesho ya Wiki ya Afya na Usalama Mahala pa Kazi yanayofanyika katika viwanja vya Mji Mwema, mjini Njombe.
Salim amesema MV Songea ni meli inayobeba abiria 200 na mizigo yenye uzito wa tani 50, na kutokana na muundo wa meli hiyo, ina uwezo wa kuingia na kutoka katika vituo 13 vilivyopo Ziwa Nyasa kuanzia Bandari ya Kiwira hadi Bandari Mbamba Bay kwa muda mfupi tofauti na meli ya MV. Mbeya II.




Amefafanua kuwa mkakati wa Serikali ni kuboresha utoaji wa huduma katika Ziwa Nyasa kwa kutumia meli mbili kwa wakati mmoja huku meli ya MV Mbeya II ikisimama katika vituo vitatu kati ya 13 hatua itakayowezesha kutumia muda mfupi kutoka Bandari ya Mbamba Bay kwenda Kiwira na meli ya MV. Songea kusimama katika vituo vyote.
Aidha, Salim ameizungumzia meli ya MV Njombe inayobeba mizigo yenye uzito wa hadi tani 1,000, akiwahimiza wafanyabiashara kutumia fursa hiyo kusafirisha bidhaa zao kwa njia ya maji.




