Serikali imepanga kuanza kutumia teknolojia ya kisasa kufuatilia uzalishaji na biashara ya madini ili kudhibiti utoroshaji na kuongeza mapato ya ndani.
Akiwasilisha bajeti ya Wizara ya Madini kwa mwaka 2026/27, Waziri wa Madini, Antony Mavunde ameomba kuidhinishiwa Sh bilioni 174.98, akisema serikali itaongeza ukaguzi wa uchimbaji, kuimarisha masoko ya madini na kudhibiti biashara haramu.
Amesema katika kuongeza uwazi, wakaguzi watatumia kofia maalum zenye kamera katika migodi ya Mirerani kufuatilia uzalishaji wa tanzanite.
Serikali pia inalenga kuongeza utafiti wa madini, kuvutia uwekezaji, kuendeleza wachimbaji wadogo na kujenga viwanda vya kuongeza thamani ya madini.
Akizungumzia utoroshaji wa madini amesema kwa kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, madini yenye thamani ya Sh bilioni 3.31 yalikamatwa katika matukio 55, ya mikoa ya kimadini.




