Ujumbe wa Tanzania umeijulisha jumuiya ya Umoja wa Mataifa kuwa nchi inazingatia misingi ya haki za binadamu kwa wananchi wote bila ubaguzi wa aina yoyote, sambamba na kuhakikisha fursa za maendeleo zinawafikia Watanzania wote kwa usawa.
Kauli hiyo imetolewa Aprili 28, 2026 katika kikao cha tano cha agenda Na. 5G cha Mkutano wa 25 wa Jukwaa la Kudumu la Umoja wa Mataifa la Watu wa Asili, kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano Na. 4, Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.
Akiwasilisha kwa niaba ya Tanzania, Mkurugenzi Msaidizi wa Haki za Binadamu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Beatrice Mpembo, ameeleza kuwa Serikali imeendelea kuweka mifumo jumuishi ya kuwawezesha wananchi kiuchumi bila kubagua wala kupendelea kundi lolote.

Amefafanua kuwa juhudi hizo zinaonekana kupitia utekelezaji wa programu na mifuko mbalimbali ya uwezeshaji ikiwemo TASAF, SIDO na AGITF, pamoja na utoaji wa mikopo kwa vijana, wanawake, wasichana na watu wenye ulemavu, hatua inayolenga kukuza uchumi shirikishi na ustawi wa jamii.
Katika kikao hicho, wawakilishi wa watu wa asili kutoka mataifa mbalimbali pamoja na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa waliwasilisha uzoefu na mapendekezo yao kuhusu namna bora ya kuimarisha ushiriki wa watu wa asili katika mifumo ya kimataifa na kikanda.
Mkutano huo ulioanza Aprili 20, 2026 unatarajiwa kuhitimishwa Mei 1, 2026, ukiwa umehusisha mijadala mbalimbali kupitia vikao vya jumla na vya pembezoni.
Mbali na mada ya uwezeshaji kiuchumi, ujumbe wa Tanzania pia uliwasilisha masuala yanayogusa haki za afya, ardhi, utamaduni, mazingira, elimu, uchumi na ustawi wa jamii.





