Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuvuka malengo ya ukusanyaji wa mapato, akisema ana imani itazidi lengo la kukusanya zaidi ya Sh trilioni 42 katika mwaka wa fedha 2026/2027.
Waziri Omar ametoa pongezi hizo wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa Ofisi ya TRA Kizimkazi, Zanzibar, ambayo itakuwa na ghorofa moja na kugharimu Sh bilioni 3.6 hadi kukamilika.


Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, amesema katika Julai 2026 mamlaka hiyo ilikusanya Sh trilioni 3.245 dhidi ya lengo la Sh trilioni 2.971, sawa na ufanisi wa asilimia 109 na ongezeko la asilimia 21.
Mwenda amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano kati ya Serikali, Bunge na walipakodi, akieleza kuwa TRA inaamini itafikia na kuvuka lengo la mwaka huu.
Aidha, amesema TRA ilikusanya Sh bilioni 325 mwezi huo na kuziwasilisha moja kwa moja kwenye mifuko 11 ya ujenzi wa miundombinu, ikiwemo barabara, maji na utalii.




