Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema hana deni na wafanyakazi wa mkoa huo kutokana na kazi nzuri wanayoifanya na kuwezesha mkoa kukua kwenye eneo la mapato.
Amesema awali mkoa huo ulikuwa unashika nafasi ya 23 kwenye eneo la mapato jambo ambalo kwasasa limebadilika na kushika nafasi ya pili ukitangiliwa na mkoa wa Dar es Salam kwa Tanzania Bara.
Amebainisha hayo katika sherehe za maadhimisho ya siku ya wafanyakazi Duniani ambapo kwa mkoa huo zilizofanyikia wilaya ya Bagamoyo.

Kunenge amesema Mamlaka ya mapato imevuka lengo walilowekewa na kwamba upande wa Mamlaka za serikali za mitaa nazo zimevuka lengo pia vipo Viwanda vya mkoa huo ambavyo vimekua na kuvuka kigezo cha kulipa ndani ya mkoa.
“Hii ndio Pwani na utendaji wenu umeonekana kila sekta tunaenda vizuri sina deni na ninyi mnafanyakazi vizuri mabadiliko yanaonekana ” amesema.
Akijibu chamgamoto za wafanyakazi Kunenge amemuagiza Katibu Katibu tawala wa mkoa huo Pili Mnyema aandae kikao na viongozi wa wafanyakazi kujadiliana kwa pamoja na mambo yatakayobainika kuwa changamoto yafanyiwe kazi.
Awali akisoma taarifa yake katika sherehe hizo Mratibu wa TUCTA Mkoa wa Pwani ambaye pia ni Katibu wa Chama cha Walimu (CWT) mkoa huo Susan Shesha amempongeza mkuu wa mkoa huo kwa kuzifanyia kazi chamgamoto zilizoainishwa mwaka 2025.
Shesha amesema madai ya walimu pamoja na kutofanyika mabaraza ya wafanyakazi ni kati ya vitu walivyokuwa wakilalamikia na serikali ya Mkoa wa Pwani imevifanyia kazi.
Katibu huyo ameomba serikali na waajiri binafsi kuongeza kiwango cha mishahara kiendane na hali ya maisha ya sasa na kuwapunguzia wafanyakazi ukali wa maisha.
Katika taarifa yake Shesha pia ameomba sheria kuchukuliwa kwa waajiri wanaowazuia wafanyakazi wao kujiunga na vyama vya wafanyakazi huku wakiwakosesha haki zao za msingi mahali pa kazi ikiwemo likizo.





