Thursday, April 23, 2026
spot_img
HomeBiasharaSpika Maulid ataka ajira kwa wazawa Kiwandani cha Rostar Tanzania

Spika Maulid ataka ajira kwa wazawa Kiwandani cha Rostar Tanzania

Imeandikwa Na Julieth Mkireri- Kibaha

Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Zubeir Maulid, amemuelekeza mwekezaji wa kiwanda cha kuunganisha magari cha Rostar Tanzania kilichopo Kerege Bagamoyo kutoa kipaumbele cha ajira kwa wazawa.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kiwanda hicho iliyohudhuriwa na viongozi wa Mkoa wa Pwani na Wilaya ya Bagamoyo, Maulid—aliyemwakilisha Rais wa Zanzibar, Hussein Mwinyi—alisema uwepo wa viwanda ni fursa muhimu ya ajira na kuongeza mapato ya taifa.

Amesema kiwanda hicho kinatarajiwa kuunganisha magari 5,000 kwa mwaka na kuhudumia masoko ya ndani na nje, ikiwemo Zambia, DR Congo, Burundi, Malawi na Madagascar, hatua itakayosaidia kupunguza uagizaji wa magari kutoka nje.

Aidha, alibainisha kuwa uwekezaji huo ni ishara ya mageuzi ya kiuchumi na fursa ya kupanua biashara kati ya Afrika na Mashariki ya Kati, huku akiikaribisha jamii ya wawekezaji kutumia mazingira rafiki ya uwekezaji nchini Tanzania.

Pia alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha mazingira ya uwekezaji.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Shaibu Ndemanga, alisema kiwanda hicho ni matokeo ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuvutia uwekezaji, kukuza uchumi na kuongeza ajira.

Alieleza kuwa Mkoa wa Pwani una viwanda vikubwa 71 vinavyosafirisha zaidi ya tani milioni 20 za bidhaa kwa mwaka, vikitoa ajira za moja kwa moja zaidi ya 22,000 na zisizo za moja kwa moja zaidi ya 62,000.

Ndemanga aliongeza kuwa serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya msingi ikiwemo umeme, maji, mawasiliano na usafirishaji ili kuvutia uwekezaji zaidi, huku akibainisha kuwa katika miaka sita iliyopita mkoa huo umepokea zaidi ya shilingi trilioni 1.561 kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Msaidizi wa Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Juddy Liu, alisema uwekezaji huo wa awali umegharimu dola milioni 20 za Marekani na unatarajiwa kuongezeka hadi dola milioni 60, huku ukitoa ajira za moja kwa moja 300 na zisizo rasmi zaidi ya 150.

Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bagamoyo, Abubakari Mlawa, amewataka wawekezaji kuweka nembo kwenye bidhaa zao ili kutambulisha eneo zinapozalishwa.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments