Friday, November 7, 2025
spot_img
HomeHabariWananchi Bunda waishukuru serikali ujenzi wa vizimba kuzuia mamba

Wananchi Bunda waishukuru serikali ujenzi wa vizimba kuzuia mamba


Wananchi wa Wilaya ya Bunda mkoani Mara wameishukuru serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajengea vizimba maalum vya kuzuia mamba, hatua iliyosaidia kuwalinda wanapochota maji, kufua, kuoga na kufanya shughuli nyingine pembezoni mwa Ziwa Victoria.

Wakizungumza leo, Oktoba 6, 2025, kwa nyakati tofauti wakati timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) ilipotembelea maeneo hayo, wananchi wamesema vizimba hivyo vimekuwa mkombozi mkubwa kwao baada ya miaka mingi ya kukumbwa na vifo na majeraha kutokana na mashambulizi ya mamba.

Mkazi wa kijiji cha Mwiseni, kata ya Butimba, Bi. Gabaseki Gervas, alisema wamefarijika sana baada ya Serikali kujenga kizimba hicho kufuatia changamoto kubwa waliyokuwa wanakutana nayo kila mwaka.

“Serikali baada ya kuona tunateseka kutokana na vifo vinavyosababishwa na mamba, ikaamua kutujengea kizimba hiki. Tunaishukuru sana Serikali na tunaomba iongeze vizimba vya ziada kwa ajili ya wanaume na mifugo,” alisema Gervas.

Naye,  Tabingwa Charles Kasao, mkazi wa kitongoji cha Nampangala, kata ya Kisorya, alishukuru Serikali kwa hatua hiyo, akisema kizimba kimeokoa maisha ya wananchi wengi, wakiwemo wanafunzi waliokuwa wakitumia ziwa hilo kwa shughuli za kila siku.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwiseni, Bw. Msiba Chiharata, alisema kutokana na manufaa makubwa yaliyopatikana kupitia vizimba hivyo, uongozi wa kijiji umeweka adhabu kwa mtu yeyote atakayeharibu eneo hilo.

“Tumeweka faini ya shilingi laki moja kwa mtu yeyote atakayeharibu au kufanya shughuli zisizoruhusiwa, ikiwemo kuanika nguo au kuingiza mifugo ndani ya eneo la vizimba,” alisema Msiba.

Msiba aliongeza kuwa vizimba hivyo vimeongeza usalama na kuondoa hofu kwa wananchi, huku akiomba Serikali kupitia TAWA kuendelea kusimamia miradi hiyo ili iwanufaishe wananchi wengi zaidi wanaoishi pembezoni mwa Ziwa Victoria.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments